Bill of Lading, Telex/Express Bill - Njoo Tukuagizie Gari

KARIBU:  NjooTukuagizieGari MDAU

YALIYOMO
Go to content

Bill of Lading, Telex/Express Bill

Fahamu kuhusu Bill of Lading, Telex Release Bill na Express Release Bill
Hizi ni hati tofauti ki mantiki lakini zipo chini ya mwamvuli mmoja ki utendaji. Hizi ni hati halali na maalumu zinazoonyesha kusafirishwa kwa mzigo zinazokuwa kama mkataba wa mtumaji mzigo na kampuni ya usafirishaji. Unapotumiwa mzigo wako kwa njia ya meli ni lazima moja ya hizi hati itumike kama utambulisho ili kuhakikisha wewe umepokea mzigo wako. Bila kuwa na hati moja kati ya hizi huwezi kutambulika kama wewe ndio mwenye mzigo na kwa hiyo huwezi kuupokea wakati utakapokuwa umefika kwenye bandari yako ya karibu. Hati hizi (documents) ki msingi hutolewa na shirika husika la meli linalosafirisha mzigo wako na hupewa muuzaji au mtumaji  wa huo mzigo atakayeufikisha huo mzigo bandarini ili kuupakia.
Hati hizi zinapotolewa, zinaeleza kuwa ndani ya vifungashio kuna nini cha aina gani na kwa idadi gani au uzito gani. Lakini kwa bahati mbaya shirika la meli linapokea tu na kuchukua maelezo ya mtumaji juu ya nini kinatumwa na kikoje ila kamwe haifungui vifungashio ili kuona na kuhakiki kilichomo. Kwa maana nyingine ni kuwa kilicho ndani ya kontena kwa mfano, hakijulikani kwa anayekisafirisha japo atakuwa ameelezwa na mtumaji na wameandika maelezo kwenye hati (Bill).
Hata hivyo usihofu kwani idara ya forodha kwa upande wa nchi unakotoka mzigo itakuwa imefungua na imejiridhisha na bado idara hiyohiyo upande wa nchi yako itafungua huo mzigo kujiridhisha, na kama itakuta tofauti na maelezo (custom declaration), utakutana na kesi nyingine inayoitwa "wrong declaration" ambapo hatua ya kwanza katika kesi hiyo ni kuuzuia (cease) huo mzigo na hatua husika zitafuata.
Katika mada hii utafahamu hati mojamoja na utaratibu wake na jinsi inavyotenda kazi. Mwisho nategemea utakuwa huna wasiwasi tena juu ya swali lolote litakalo ibuka juu ya masuala hayo.
Original Bills of Lading
Hii ni hati au kibali cha kusafirisha mzigo kwenda nchi nyingine. Hutolewa tu pale mzigo unapopakiwa kwenye meli na anayehusika kutoa ni shirika la meli husika. Kama nilivyoeleza hapo mwanzo ni kwamba huwezi kupokea mzigo bila kuwasilisha nakala halisi (Original Bill of Lading) wakati wa kupokea.
Wakati mwingine kama hamjamalizana ki malipo, kwa kutumia kigezo hicho muuzaji anaweza akaizuia nakala halisi asikutumie hadi umalizie kumlipa hela zake ndipo akutumie kwani bila nakala halisi kupokea mzigo wako ni ndoto.
Telex Release Bills of Lading
Hapa kama ilivyo kawaida, shirika la meli litatoa kibali/hati halisi (Original Bill of Lading) pale tu mzigo ukipandishwa kwenye meli. Ila tofauti hapa ni kuwa, baada ya mtumaji kupewa hiyo hati anaweza kukaa hata siku tatu akaamua kuirudisha (surrender) hiyo hati kwa shirika la meli. Kisha shirika hilo la meli litaitaarifu kwa njia ya kielektoniki ofisi yao iliyo upande wa nchi yako unayopokelea mzigo kwamba mtumaji amerudisha nakala halisi ofisini upande wa kule mzigo unakotoka.
Kisha ofisi ya meli kutoka kule mzigo utokako watagonga mhuri "TELEX RELEASE" juu ya hiyo hati na kumpatia tena mtumaji. Mtumaji ataituma hiyo hati kwa njia ya kielektroniki mfano barua pepe au nukushi kwa mpokeaji wa huo mzigo. Kwa hivyo mpokeaji akipata hiyo nakala kwa njia ya barua pepe au nukushi yenye mhuri "TELEX RELEASE" ataweza kupokea bila ulazima wa kuwa na nakala halisi (Original Bill of Lading)
Hii aina ya hati ni nzuri hasa linapokuja swala la uharaka wa kutoa mzigo bandarini au muuzaji kupokea pesa zake haraka. Hii hufanyika mara nyingi katika soko la alibaba ambapo muuzaji hulipwa kwa njia ya escrow na hapati pesa bila kuhakikisha nakala zimemfikia mnunuaji. Kwa hiyo hutumika sana kwa uhitaji wa haraka.
Express Release Bills of Lading
Hii hati ndio njia rahisi na ya haraka zaidi ya zote kwani mtumaji kamwe hatopewa nakala halisi na hivyo hahitajiki kuirejesha kwa ofisi ya meli na wala mpokeaji hana haja ya kupeleka nakala halisi anapoenda kupokea mzigo wake. Shirika la meli litamtumia muuzaji/mtumaji hati kwa njia ya kielektroniki mfano barua pepe au nukushi kisha nae atamtumia mnunuzi/mpokeaji wa mzigo kwa njia hiyo hiyo ya kielektroniki.
Natumaini umefahamu aina za hizi hati na jinsi zinavyotumika. Mara nyingi sana wauzaji hutumia Original Bill of Lading kwa sababu ni haki na ni uchaguzi wake lakini wewe mnunuaji si mbaya na huzuiwi kuomba hati zako uzipate katika mfumo upi kati ya tatu hapo juu.
Pia hati hii hutumwa pamoja na hati zingine zinazohusiana na mzigo huo kama vile risiti ya manunuzi, hati ya bima, kibali cha kusafirisha toka wizara husika na hati ya ukaguzi wa huo mzigo kuna mada ambayo utajifunza umuhimu wa ukaguzi wakati wa kuuza bidhaa nje (export) na/au kununua nje ya nchi (import) na utajifunza na kujua mashirika yenye dhamana ya kimataifa ya kufanya ukaguzi. Hati hizo za ziada nilizotaja zinaweza kuwa zote au baadhi yake lakini kamwe Bill of Lading haitumwi peke yake.

MAKAO MAKUU

Quality Plaza, 2nd Floor, West Wing, Room No. 346
Nyerere Road, Dar es Salaam
S.L.P 100047
+255 684 454 441
+255 713 416 275
www.kalumbilo.co.tz

            Mawasiliano ya haraka
Whatsapp na Barua pepe
Za jumla [General] 0713 416 275
                                     0684 454 441
          Mwanza Pekee:     0767 251 237
          Mbeya Pekee:       0629 822 276


Email:  service@kalumbilo.co.tz
© 2015-2020 Kalumbilo Imports & Commission Agency Co. Ltd  
Back to content